Thursday, July 23, 2009

Ni zamu ya Joshua John Mlelwa kung'ara






(Joshua John Mlelwa akiwa kwenye jukwaa pamoja na Kundi la Kijitonyama Upendo Group katika moja ya matamasha ya Injili yaliyofanya nchini Tanzania.

Na Mdau wetu

MAKUNDI mengi ya muziki wa Injili nchini Tanzania yamekuwa ni nguzo muhimu katika kulea vipaji vya waimbaji wengi wa muziki huu. Joshua John Mlelwa ni miongoni mwa vipaji vingi hapa nchini vilivyokulia kwenye mikono ya kundi.
Kabla ya kutoka kama muimbaji binafsi, Joshua amekuwa kwenye Kundi la Kijitonyama Upendo Group (KUG) tangu mwaka 1999.
Kabla ya kuwemo kwenye kundi hilo Joshua alikuwa akiimba kwenye Kwaya ya Vijana ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Usharika wa Sumbawanga mwaka 1992 na wakati huo alikuwa akisoma shule ya sekondari ya Mazwi iliyopo mkoani Rukwa.
Baadhi ya kazi alizofanya pamoja na KUG ni pamoja na Mungu Anakupenda ambayo ilikuwa ni albamu yenye nyimbo tisa ndani yake ambazo ni Haleluya, Njooni Kwangu, Tutapataje Kupona na nyingine nyingi.
Pia waliweza kutoa albamu iitwayo Maombolezo iliyokuwa na nyimbo nane, na hii waliitoa wakati wa kifo cha Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, iliyokuwa na nyimbo kama Taifa Lako Lakulilia, Tutakukumbuka sana pamoja na Mbona Mapema.
Licha ya kupata mafanikio hayo akiwa ndani ya Kijitonyama Upendo Group, ametoka na albamu mbili. Albamu ya kwanza ameitoa mwaka 2007, iitwayo Yesu Yupo yenye vyimbo nane ambayo ameitoa maalum kwa ajili ya kituo cha kulelea watoto Yatima cha Hananasifu Wilayani Kinondoni jijini Dar es Salaam.
“Unajua ukitaka kufanikiwa ni lazima uhakikishe kuwa unakuwa mtoaji ndiyo maana mimi na mke wangu tuliamua kuwa watoaji kwa kutoa albamu hii kwa gharama zetu na mauzo yote kukiachia kituo hicho bila kuchukua hata shilingi moja,” ameongeza muimbaji huyo.
Baada ya kutoka na albamu ya kwanza Joshua Mlelwa ametoka na kazi mpya iitwayo Shaloom yenye nyimbo nane ambazo ni Shaloom, Apewe Sifa Bwana, Niko Juu, Heri Niwe na Wewe pamoja na nyingine nyingi.
“Baada ya albamu ya kwanza hivi sasa nimeshatoa albamu ya pili iitwayo Shaloom na kazi hii nimeifanya ndani ya studio za Shekinah za jijini Dar es Salaam na itakuwa mtaani juma hili,” amefafanua muimbaji huyu mkongwe kwenye muziki wa Injili.
Juu ya mwelekeo wa Muziki wa Injili hapa nchini Joshua ametanabaisha kuwa mwelekeo si mbaya ila wapo baadhi ya waimbaji wa muziki huo wanaoufanya bila kuwa na hofu ya Mungu.
“Watu wanaimba bila kuwa na hofu ya Mungu, wanafanya hivi kwa kuwa wana kipaji lakini hii si sababu ya kuwa mwimbaji wa Injili kwani muziki huu unafanywa kwa ajiliya Mungu. Kwa mfano, hata Michael Jackson amekuwa maafuru ulimwenguni kutokana na kipaji chake cha kuimba lakini hakuwa na hofu ya Mungu, ” amefafanua Joshua ambaye ni baba wa mtoto mmoja.
Kuhsu suala la wizi kwenye sanaa ya Tanzania kwa ujumla, Joshua amesema kuwa ili kulikomesha tatizo hili ni kwa wapenzi wa sanaa kuachana na tabia ya kununua bidhaa bandia na wasanii kuwa na umoja na kushirikiana.
“Wizi bado ni tatizo, kwa mfano nchi nyingi za Afrika Mshariki na Kusini wanatufahamu vema kutokana na kazi zetu ambazo mapato yake hatuyaoni kwa sababu ni kazi za kunakili kutoka kwenye ‘original’,” amesema Joshua.
Baadhi ya nchi ambazo kazi za Kijitonyama Upendo Group zinauzwa kinyemela bila kuwanufaisha ni Malawi, Zambia, Kenya, Botswana, Kenya, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Burundi na Rwanda.

3 comments:

Anonymous said...

tunaingojea albam hiyo kwa mikono miliwi sasa lini?

Anonymous said...

hongera kaka au ndiyo unaondoka kijitonyama?
naitwa eric nipo hapa London UK

wazalendomedia.com said...

huyi mtumishi kazi zake zinakubalika sana naomba kujua ni vipi ataweza kutufikia hata sisi? tuliopo nje ya Tanzania?.

mimi naitwa criss Macha nipo CAPETOWN Afrika kusini na nimekuwa nikiziona kazi za Upendo Group kwa wauzaji hasa Botwasa ambapo natembelea mara kwa mara nikifanya kazi zangu za kibiashara.