Update:
Nyumba ya Mkuchika inawaka moto-Newala
Taarifa za redio mbao sasa ni kwamba wananchi wanaendelea kufanya uharibifu mkubwa huko ambapo naambiwa wamevamia gereza wakafungulia wafungwa na kisha kupiga moto gereza. Polisi wamezidiwa na wamejifungia kituoni wanarusha mabomu yao tokea huko walikojificha maana nje hakutamaniki. Na wameshateketeza nyumba ya mama Anna Abdallah.
Update:
Kikao cha dharura cha kamati ya ulinzi na usalama kinaendelea kwa kuwashirikisha maafisa wa polisi na maafisa usalama waliotoka Dar es Salaam kuongezea nguvu.
Maaskari na makachero wawasili Mtwara leo asubuhi na helkopta kuongezea nguvu.
Hosteli ya wanafunzi wa chuo cha Utumishi maeneo ya Kiyangu B Mtwara yakoswa koswa kuchomwa moto kwa kile kinachodhaniwa kuwa na uhusiano na Hawa Ghasia mpaka sasa wanafunzi hawana mahala pa kukaa. Kituo kidogo cha Polisi Cha Shangani mkoani Mtwara nacho chakoswa na moto. Ofisi ya Afisa Mtendaji Nkanaledi mkoani Mtwara nayo yavunjwa.
Wananchi wamechoma moto mahakama ya Mwanzo na kuvunja vioo vya nyumba za waheshimiwa Hawa Ghasia (Waziri, TAMISEMI) na ya Mohamed Sinani (Mwenyekiti wa CCM Mkoa) zilizopo mtaa wa Sinani.
Wakiwa katika mahakama ya mwanzo, Polisi walizingirwa na vijana waliokuwa wamebeba mawe na kufunga barabara zote za kuingia na kutoka Kituo Kikuu cha Mabasi na eneo la Soko Kuu, licha ya kufyatua hewani mabomu ya machozi.
Baadhi ya barabara za zimezibwa kwa kuchomwa matairi ya gari, na kuongeza hofu kwa wananchi.
POLISI jana wamelazimika kupiga mabomu ya machozi kutwa nzima katika kata ya Chikongola, Manispaa ya Mtwara Mikindani kutawanya wananchi walioizingira nyumba ya diwani wa kata hiyo Mohamedi Chehako kwa madai ya kuwahifadhi wachawi ndani ya nyumba yake, huku mwandishi wa habari mmoja akiripotiwa kujeruhiwa.
Habari ambazo hazijathibitishwa na kamanda wa polisi mkoani hapa, Maria Nzuki zinadai kuwa majira ya saa 10 kasoro za jioni watu wanaodaiwa kuwa ni wanajeshi wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) waliingilia kati na kuanza kutembeza mkong’oto kwa wananchi ili kuzima vuguvugu hilo.
Mwandishi wa habari hizi alipojaribu kuwasiliana na kamanda Nzuki kwa njia ya simu za mkononi hakuweza kupatikana.
Wananchi walitoa tuhuma hizo baada ya kukuta ungo ikiwa na tunguri ndani yake ambayo inadaiwa kuwa ni ndege ya wachawi uwanjani kwake maeneo ya makaburi Msafa.
Wananchi walijikusanya nyumbani kwa Diwani huyo na kumshinikiza awatoe wachawi nje ili waweze kuwadhibu, amri iliyopingwa na Diwani huyo. Kadiri mda ulivyokwenda ndivyo wananchi walivyozidi kuongezeka na hatimaye kulijitokeza kundi la watu walioanza kutia vurugu, hali iliyomlazimu Chehako kuomba msaada wa polisi.
Mashuhuda wa tukio walimweleza mwandishi wa habari hizi kuwa polisi walipofika waliwasihi wananchi kutawanyika kwa kuwa ungo na tunguri zake zilikuwa zimeteketezwa kwa moto na diwani huyo mbele ya wananchi hao.
Chehako akihojiwa nyumbani kwake alisema: “Wananchi waliendelea kupinga na kudai ndani ya nyumba kuna rubani na abiria wa ndege nimewahifadhi…polisi wakawachagua wananchi watano na kuingia ndani ya nyumba kuwasaka watu hao…hawakuona kitu, walitoka nje na kuwamabia wenzao hata hivyo wenzao walibisha.
Walianza kurusha mawe nyumba… polisi walianza kupambana nao kwa kuwarushia mabomu…hata hivyo wananchi walikuwa wanakimbia na kwenda upande wapili kufanya vurugu.”
Chehako alibainisha kuwa ni kawada yake kuamka alfajiri kwa ajili ya sala ya asubuhi, lakini asubuhi ya jana alishindwa kuamka mapema, hata hivyo hakuweza kuhisi jambo lolote: “Ilipofika saa 12 asubuhi nikaanza kusikia watu wakishangaa kitu nje, nilipotoka nikakuta nyungo na tunguri ndani yake…mara wakaja vijana wawili na pikipiki wakachukua ule ungo na kukimbia nao…nikawatuma vijana wawafuate waurudishe…walifanikiwa na nyungo ile ilirejeshwa nyumbani hapa na ndipo nilipouteketeza kwa moto.
Nilidhani yatakuwa yameisha, lakini wananchi waliendelea kudai nimewafungia wahuska ndani, si kweli hakuna mtu humu ndani wala mimi sijui kilichotokea hadi hivyo vitu vikawa humu ndani.”
Katika mapambano hayo ya wananchi na polisi, wananchi kwa kutumia mawe wamemjeruhi Mwandishi wa Habari wa Channel Ten mkoani hapa, John Kasembe kwa jiwe kichwani, sehemu za kisogoni ambapo ametibiwa zahanati ya Fajima na anaendelea vizuri.
Kwa mujibu wa Kasembe, alipigwa mawe kichwani akiwa kazini kukusanya habari na wananchi waliokuwa wakiwarushia mawe polisi.
Ofisa wa polisi ambaye jina lake hakutaka litajwe kwa sababu si msemaji wa jeshi hilo amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kuongeza kuwa gari moja ya polisi PT 1421 limevunjwa kioo cha mbele kwa mawe.
Hadi saa 10.00 jioni bado polisi walikuwa wanaendelea kupiga mabomu ya machozi hewani huku wananchi wakionekana kujipanga katika makundi hali iliyotishia usalama wa maeneo hayo.
Hii ni kwa mujibu wa www.mtwarakwetu.blogspot.com