Friday, August 26, 2011

Uuzwaji wa mahakama mazungumzo yaendelea



Na Veronica Kazimoto – MAELEZO

DAR ES SALAAM

Mazungumzo bado yanaendelea kati ya Serikali na Muwekezaji aliyejitokeza kununua jengo la Mahakama ya Rufani iliyopo katika makutano ya barabara ya Kivukoni na Ohio jijini Dar es Salaam.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Celina Kombani wakati akijibu hoja mbalimbali za wabunge waliokuwa wakichangia hotuba ya makadirio ya bajeti ya wizara hiyo.

“Kuhusu suala la uuzwaji wa jengo la Mahakama ya Rufani, mazungumzo baina ya Serikali na muwekezaji aliyejitokeza bado yanaendelea hivyo basi napenda kuwatoa hofu waheshimiwa wabunge kuhusiana na suala hili,” amesema waziri Kombani.

Waziri Kombani amefafanua kuwa mazungumzo yanaendelea baina ya muwekezaji na ofisi mbalimbali za Serikali kama ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mahakama ya Rufani,Wizara ya Maliasili na Utalii, Wizara ya Katiba na Sheria na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.

Aidha, Waziri Kombani amesema muwekezaji aliyejitokeza ameahidi kujenga mahakama ya Rufani yenye hadhi kulingana na umuhimu waka kama mhimili mojawapo wa dola.
Kama muafaka utafikiwa kati ya muwekezaji na Serikali jengo hilo la Mahakama ya Rufani litajengwa maeneo ya mtaa wa Chimala mkabala na barabara ya Taasisi ya Saratani ya Ocean Road.

Hivi karibuni vyombo mbalimbali vya habari vimekuwa vikitoa taarifa kuhusiana na jengo la Mahakama ya Rufani kununuliwa na muwekezaji wa hoteli ya Kempinski na kuwa sehemu ya hoteli hiyo kwa ajili ya maegesho ya magari.

0 comments: