TUZO za Wazalendo 2012, zinatarajiwa kufanyika
Januari 31 mwaka 2013 jijini Dar es Salaam badala ya Desemba 30 mwaka huu kama
ilivyotangazwa hapo awali.
Mratibu wa tuzo hizo, Ahadi Kakore alisema kuwa
kwamba sababu za kusogezwa mbele kwa fainali hizo ni kutoka Desemba 30 hadi Januari
31 ni kutokana na baadhi ya mambo kutokamilika kwa wakati, ingawa bado
zitafanyika ndani ya jiji la Dar es Salaam.
Aidha sababu nyingine ni kwamba wanakamati wengi
wamekuwa kwenye pilikapilika za uchaguzi wa Chama cha Makocha Tanzania (Tafca)
kwa sababu wengi wao ni wanachama hivyo jambo ambalo limesababisha kushindwa
kutekeleza baadhi ya mipango yao kwa wakati.
“Zipo sababu nyingi lakini kubwa ni kwamba baadhi
ya wageni muhimu ambao walialikwa asilimia (80%) wameonyesha kutokuwepo kwa
tarehe hiyo kwa sababu watakuwa nje ya jiji la Dar es Salaam kwa ajili ya siku
kuu za mwisho wa mwaka.
“Kwa kuzingatia uzito wa jambo lenyewe kamati
imeona ni busara kusogeza mbele kwa siku 30 kwa lengo la kuwapa nafasi wahusika
kwa pande zote mbili kuendelea na matayarisho hayo,” alisema Kakore.
Katika hatua nyingine, majina ya wanasoka
walioingia fainali ya tuzo za mwakasoka bora wa mwaka yanatarajiwa kuwekwa wazi
Januari mosi mwaka huu baada ya kukamilishwa kwa mchakato wa kupitia majina 93
yaliyokuwa yamependekezwa na wadau wa soka.
Mchakato wa
kumpata mwanasoka bora wa mwaka ulianza tangu Agosti mosi mwaka huu ambapo
wadau mbalimbali wa ndani ya nje ya Tanzania walipendekeza majina ya wachezaji
ambao walistahili kutwaa tuzo hiyo.
Tuzo za Wzalendo
zinalenga katika kuinua na kutambua mchango wa maendeleo ya soka la Tanzania
kwa kipindi cha mwaka wa 2012 ambapo zitakuwa zikifanyika kila mwaka lengo
likiwa ni kuendeleza na kuthamini kazi ambazo zimefanywa na wanasoka na wadau
wa soka kwa muda wa mwaka mmoja.
0 comments:
Post a Comment