Thursday, July 23, 2009

GAMA WAUSHUKIA MUZIKI WA INJILI




MNENDO wa muziki wa Injili kukubalika kwa mashabiki na wapenzi wake kwa sasa unachangiwa na mambo mbalimbali ambayo ni uimbaji, utunzi na utayarishaji ulio bora.
Gamaliel Daniel Mwasumbi ni miongoni mwa waimbaji ambao wamewezesha suala la uimbaji Tanzania kubadilika na kuwa wa aina yake kwa kuwa wakati anaanza kazi hii yeye na wenzake, Godwin Gondwe na David Robert waimbaji binafsi walikuwa wachche hivyo kujikuta wakiwa na mzigo wa kuhakikisha injili inawafikia watu wengi zaidi.
Katika mazungumzo yake na mdau wa tanzaniacelebrity.com Gamaliel ambaye wengine wanamtambua kama Gama anasema kuwa kwenye huduma hii ya uimbaji baadhi ya mambo hayaendi sawa hivyo kuna haja ya kuwa na neon la uponyaji kwa ajili ya waimbaji na watayarishaji wa muziki wa Injili.
Mambo ambayo Gama anayaona kama ni kikwazo kwenye muziki wa Injili ni pamoja na baadhi ya waimbaji kufanya huduma ya Injili kwa kulenga pesa badala ya kumtumikia Mungu kama ilivyokuwa hapo awali.
“Misingi ya awali kwenye uimbaji wa nyimbo za Injili umevunjwa, kwa maana zamani uinjilisti kwa njia ya uimbaji ilikuwa ni kazi ya wito lakini kwa sasa nashangaa eti muimbaji anaitwa mahali anaanza kuweka masharti mbalimbali ikiwemo suala la kutaka kulipwa,” amesema muimbaji huyo.
Kadhalika Gama ameelezea juu ya utunzi bora wa mashairi kwa kusema kwamba muziki wa Injili si mipasho hivyo waimbaji wanatakiwa kutunga nyimbo zitakazookoa roho za watu kwani hiyo ndiyo kazi ya muziki huo katika jamii.
Amefafanua kuwa kamwe Mungu hana hasara kwa maana amejitosheleza na hivyo kama watu watashindwa kuimba katika roho na kweli ataendelea kuwa Mungu.
“Waimbaji tuzingatie huduma kwa kutunga nyimbo zitakazoweza kuokoa roho za watu kwani bila kufanya hivyo mwisho wa siku tutadaiwa, lakini ninachopenda kuongezea ni kwamba kamwe Mungu hana hasara kama tukiacha kumuimbia, vile vile tusiimbe mipasho,” ameongeza Gama.
Wakati huo huo Gama ameeleza kuwa watengenazaji wa muziki huo kwenye studio (producers) wamekuwa hawaangalii ubora bali fedha imekuwa ni kichocheo kikubwa katika kufanya kazi, jambo linalochangia kutoa kazi zilizo chini ya kiwango.
Licha ya hali hiyo Gama ameongeza kuwa baadhi ya watangazaji kwenye vituo vya redio na televisheni za Kikristo wamekuwa wakiendekeza vitendo vya rushwa kwa waimbaji jambo linalosababisha wale wasiokuwa na uwezo wa kifedha kazi zao kushindwa kusikika kikamilifu.
Gama ambaye kwa sasa anakuja na albamu ya peke yake baada ya kufanya kazi na waimbaji wenzake kwenye Kundi la Yahweh Music linaloundwa na David Robert, Godwin Gondwe pamoja na yeye Gama, amesema kuwa kazi yake hii itakuwa ni tofauti kutokana na kujaza vionjo vya sehemu mbalimbali duniani.
“Albamu yangu mpya itakuwa na mchanganyiko wa vionjo vya Kihindi na Kisenegal na imepewa jina la Usinipite na ina jumla ya nyimbo 12 ambazo ni Mwenye Enzi, Mungu Mkuu, Tunakutukuza, Usinipite, Usisahau, Amen na nyingine,” ameeleza Gama.
Kabla ya kutoka kivyake Gama aliyekuwa kwenye Kundi la Yahweh Music yeye na wenzake walitoa na albamu iitwayo Baba iliyotoka mwaka 2003 na ilikuwa imebeba jumla ya nyimbo 10 ambazo baadhi yake ni Baba, Haleluya Hosana, Nakupenda, Bwana Atafanya Njia na nyinginezo nyingi.
Baadaye alienda jijini Nairobi nchini Kenya akifanya shughuli za muziki wa Injili pamoja na masomo na hivi sasa amerejea nyumbani akiwa na mke aitwaye Rose Boke pamoja na mtoto mmoja wa kiume aitwaye Ntimi.
“Napenda kuwashukuru wadau mbalimbali waliowezesha mimi kufika hapa na wanaendelea kukuza muziki wa Injili hapa nchini, nao ni Eric Shigongo Mkurugenzi wa Global Publishers, vyombo vya habari pamoja na wadau wengine,” amesema Gama.

0 comments: