Monday, July 20, 2009

Jinsi Maxell alivyotua Barca

Barcelona, Hispania

Harakati za usajili wa Ligi Kuu nchini barani Ulaya zinaendelea ambapo kumekuwepo kwa taarifa za hapa na tale juu ya uhamisho wa wanasoka kutoka klabu moja na kwenda klabu nyingine.

Kwa muda sasa klabu ya Barcelona mabingwa wa Ligi ya Hispania ‘La Liga’ ambao pia ni mabingwa wa Ulaya, wamekuwa katika mbio za kuweza kumnasa mlinzi wa pembeni wa kutoka klabu ya Inter Milan huku mengi yakisemwa juu ya mbio hizo.


Lakini pamoja na maneno na minong’ono mingi hatimaye wiki iliyopita mabingwa hao waliweza kunasa saini ya Maxwell Scherer Cabelino Andrade anayecheza nafasi ya ulinzi na kiungo.

Maxwell raia wa Brazil amekuwa ni miongoni mwa wachezaji waliotingisha usajili wa Ulaya kutokana na mvutano ambao ulianza jitokeza baada ya Barcelona kutoa taarifa za kumtaka.

Mchezaji huyo inasemekana kuwa anachukua nafasi ya Sylvinho, anayetarajiawa kutua kwenye klabu ya Deportivo La Coruna kufuatia kuanza mazungumzo ya chini kwa chini kati ya klabu hiyo na Barcelona.


Hata hivyo taarifa kutoka ndani ya klabu ya Barca zilisema kuwa klabu hiyo na Inter Milan wamekubaliana katika masuala yote ya uhamisho na ndiyo sababu ya mlinzi huyo kusaini mkataba wakali hao wa Camp Nou na ameshatambulishwa kwa mashabiki wa klabu hiyo ya jijini Barcelona.

Uhamisho wa Maxwell Scherer Cabelino Andrade umeigharimu Barcelona kiasi cha Pauni za Uingereza milioni saba, huku mlinzi huyo akionekana mwenye furaha kuujiunga na wakali hao wa Ulaya.

“Hii ni hatua mpya katika historia ya maisha yangu, nimekuja hapa lakini nikiwaacha marafiki, mashabiki wangu Inter Milan lakini sina budi kukubaliana na hali ya dunia, ila ninachoomba kutoka kwa mashabiki wa soka ni umoja, upendo mshikamano na mimi nitafanya kazi kwa nguvu na juhudi zote,” amesema mkali huyo.

Baadhi ya wadadisi wa masuala ya soka nchini Hispania wanasema kuwa Maxwell (27) anaweza kuwa nguzo muhimu kwenye maendeleo kwenye klabu hiyo Barcelona ambayo kwa sasa wameshikilia mataji matatu makubwa ambayo ni Kombe la Ulaya, Ubingwa wa La Liga na Copa del Rey.

Klabu ya Real Madrid ndiyo inayotingisha dunia kwa sasa kwenye usajili kufuatia kutenga kitita cha Pauni za Uingereza milioni 200 ili kufanikisha zoezi hilo huku ikifanikiwa kumtwaa Ricardo Kaká, Raul Albiol, Cristiano Ronaldo na Karim Benzema.

Maxwell Scherer Cabelino Andrade alizaliwa Agosti 27 mwaka 1981 katika eneo la Vila Velha nchini Brazil.

Kabla ya kutua Barcelona alikuwa akikipiga kwenye klabu ya Inter Milan ambao ni mabingwa wa Ligi Kuu ya Italia (LIGUE) akicheza nafasi ya mlinzi wa kulia pamoja na kiungo, pia amezitumia timu za Cruzeiro, Ajax, Empoli.

0 comments: