Tuesday, July 31, 2012

Man Utd yachafuka fedha


LONDON, England

KLABU ya Manchester United, imeingia mkataba wa miaka saba na Kampuni ya kutengeneza magari ya nchini Marekani ya General Motors ambao utaanza kufanya kazi rasmi katika msimu wa mwaka 2014/15.

Mkurugenzi wa biashara wa klabu ya Manchester United, Richard Arnold, alisema kuwa ni moja ya mafanikio kupata mkataba wa muda mrefu ambao utakuwa na manufaa makubwa kwa klabu.

“Hili ni jambo jema kupata mkataba wa muda mrefu kiasi hiki. Tulikutana na Chevrolet kwa muda wa wiki sita tu, lakini waliweza kufanya jambo kubwa kiasi hiki ambalo lina faida kwa pande zote ambao utasaidia kuwafikia mashabiki wetu zaidi ya milioni 659 kote duniani.

Kwa upande wake, Alan Batey,  kutoka kampuni ya General Motors kwa upande wa Marekani ya Kaskazini,  alisema kwamba wamefurahi kuunganisha watu duniani kwa kutumia Manchester ambapo bidhaa yetu ya Chevrolet itafikia watu wengi zaidi.

“Kwa mwendo huu naamini tunaweza kuwafikia mashabiki wengi zaidi, lakini pili bidhaa yetu inaweza kuwafikia watu wengi zaidi duniani, tofauti na awali ambapo tusingeweza kufika kutokana na sababu mbalimbali.

“Tunajua kwamba chini ya uongozi wa Alex Ferguson tunaimani kubwa kwamba bidhaa yetu itawafikia watu wengi kwa ukaribu zaidi,” alikaririwa bosi huyo.

Mkataba huo ni wa kitita cha pauni milioni 210 ambazo ni zaidi ya Sh bilioni 525, ambao utafunika wa sasa na Kampuni ya AON.

Kutokana na tangazo hilo, imefanya kuongezeka kwa nguvu ya hisa kwenye soko la kimataifa la hisa la Marekani jambo litakalowezesha kuvutia wanahisa wengi.

Aidha kiasi cha pauni milioni 30 ndicho kitakachokuwa kinatolewa kwa mwaka kwa ajili ya kuchapisha jezi za klabu hiyo kila msimu, ambapo sasa imevuka ule wa mabingwa wa zamani wa Ulaya Barcelona Qatar Foundation, ambapo inatumia kiasi cha pauni milioni 25 kwa mwaka kwa ajili ya machapisho ya jezi kila mwaka.

Mkataba wa sasa wa Manchester United  na AON (jezi mpya pichani) unafikia kiasi cha pauni  milioni 20 kwa mwaka huku ule wa awali na AIG  ulikuwa wa pauni milioni 14 kwa mwaka hali inayoonekana kukua kwa mtaji kila mkataba na kampuni mpya.

Kutokana na  mkataba huo huenda inaongeza nguvu kwenye mikakati yake ya usajili ambayo imelenga kuwasajili, Robin van Persie  kutoka Arsenal  kwa dau la pauni milioni 15 huku Mbrazil Lucas Moura (19) kutoka klabu ya Sao Paulo ya Brazil kwa gharama ya pauni milioni 30. 
Man United na jezi mpya.

0 comments: