Diwani kata ya MWIMBI wilaya MPYA ya KALAMBO Mkoa wa Rukwa Leonard
Shalamwana (wa tatu kulia)akimuonesha Mkuu wa wilaya Moshi Mussa
Chang'a(wa tatu kushoto) chanzo cha Mradi wa maji utakaogharimu zaidi ya
shilingi milioni 158.3 na kunufaisha takribani wakazi 8,000. Mradi huo
unadhaminiwa na benki ya dunia, wananchi pamoja na mfuko wa maendeleo wa
jimbo la Kalambo. Wengine kutoka kushoto ni Mratibu wa Miradi ya TASAF
wilaya John Kiondo na Kaimu Mkurugenzi wilaya Sumbawanga Crispin Luanda.
NA RAMADHANI JUMA,
AFISA HABARI, SUMBAWANGA
WAKAZI wapatao 8,000 wa vijiji viwili vya Majengo na Mwimbi
katika Kata ya Mwimbi wilaya mpya ya Kalambo Mkoa wa Rukwa wanatarajia
kunufaika na mradi wa maji safi
unatekelezwa katika kata hiyo kwa gharama ya zaidi ya shilingi milioni 158.3.
Mradi huo unadhaminiwa na Benki ya Dunia iliyotoa zaidi ya
shilingi milioni 154.4, wakazi wa kata hiyo wamechangia shilingi 2,709,000 na
mfuko wa jimbo la Kalambo umetoa shilingi 1,200,000 ili kufanikisha mradi huo.
Akielezea mradi huo mbele ya Mkuu wa wilaya ya Kalambo Moshi
Mussa Chang’a, diwani wa Kata ya Mwimbi Leonard Shalamwana alisema kwa sasa
mradi huo uko katika hatua ya nne ambayo ni usambazaji wa maji katika vituo
vikuu.
Afisa Mtendaji wa Kata hiyo Mosses Nkinda alisema mradi huo
utaongeza upatikanaji wa maji kwa wakazi hao na kuongeza kasi ya maendeleo na
kukuza hali ya kiuchumi mara utakapokamilika.
Kwa upande wake, Mkuu wa wilaya hiyo Moshi Mussa Chang’a
alipongeza utekelezaji wa mradi huo na kuwataka viongozi wa kata hiyo
kuhakikisha kuwa unakamilika haraka ili wakazi hao waanze kunufaika nao kama ilivyokusudiwa.
0 comments:
Post a Comment