Habari zote na Juma Mohammed, MAELEZO Zanzibar
Kukosekana kwa uzalendo na tama ya kipato kikubwa kumetajwa
kuwa sababu ya ya baadhi ya wananchi wataalam kuacha kazi Serikali ya Mapinduzi
Zanzibar na kukimbilia ughaibuni.
Akijibu swali katika Baraza la Wawakilishi, Waziri wa Nchi
Ofisi ya Rais Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Haji Omar Kheri alikiri kuwepo
kwa tatizo la wataalam wa kizalendo kuondoka nchini kwa kutafuta maslahi zaidi
nje ya nchi.
Katika swali la
msingi,. Mwakilishi wa Jimbo la Wawi
(CUF) Saleh Nassor Juma alitaka kujua sababu za wataalamu kuendelea kukimbia
nchini.
Mwakilishi huyo apamoja na Mwakilishi wa Salum Abdallah
Hamad (CUF) wa Matambwe, Rashid Seif Suleiman (CUF) wa Ziwani na Jaku Hashim
Ayoub wa Jimbo la Muyuni (CCM) wote walilalamika kuwa serikali inachangia
kuwatorosha wataalamu kwa kuwawekea mazingira mabaya ya utendaji kazi na malipo
duni.
“Naomba nikubaliane na wajumbe wa baraza la wawakilishi kuwa
nchi nyingi zilizopo kwa janga la sahara hukimbiwa sana na wataalamu wake hususan madaktari
wakiwemo pia maprofesa na wahadhiri licha ya kulipwa stahiki mbali mbali”
alisema waziri Kheri.
Waziri alisema Zanzibar
pia imekuwa ikikabiliwa na tatizo la kukimbiwa na wataalamu wake hasa kada ya
udaktari hospitali ambao wanakwenda nchi nyengine kupata maslahi mazuri zaidi.
Hata hivyo waziri huyo alisema miongoni mwa sababu
zinazosababisha wataalamu kukimbia ni ukosefu wa maslahi bora na vitendea kazi
lakini kubwa zaidi ni kukosa uzalendo.
“Serikali imekuwa ikifanya juhudi za kuimarisha maslahi ya
watumishi wake na kuanzia mwaka jana wataalamu mbali mbali walirekebishiwa
mishahara pamoja na posho wakiwemo madaktari lakini licha ya hilo kutokana na kukosekana uzalendo baadhi
ya madaktari wanaondoka” alilalamika waziri huyo.
Waziri Kheri aliwataka wajumbe wa baraza la wawakilishi
kusaidia katika juhudi za kuwashawishi wataalamu waliokuwepo nchini kupenda
nchi yao na
kuwatumikia wananchi huku serikali ikifanya juhudi za kuimarisha maslahi na
mazingira bora ya kazi.
0 comments:
Post a Comment