Na Mwandishi Wetu
RATIBA ya
michuano ya Kombe la Kagame inatarajiwa kutolewa Ijumaa ijayo jijini Dar es
Salaam ikiwa ni maandalizi ya michuano hiyo mikubwa kwa ngazi ya klabu katika
Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.
Katibu Mkuu
wa Baraza la vyama vya soka Afrika Mashariki Kati, (Cecafa) Nicholas Musonye amesema kwamba, kabla ya kutolewa kwa ratiba
hiyo itafanyika droo ya kupata makundi.
Aidha katibu
huyo amesema kuwa, wanachosubiri hivi sasa ni uthibitisho wa klabu ya El
Merriekh ya Sudan pekee, ambayo awali ilikuwa kwenye hatihati ya kutoshiriki
michuano hiyo kutokana na sababu mbalimbali.
“Tunasubiri
El Merreikh ambayo inatakiwa kuthibitisha ushiriki wao kwani klabu karibu zote
zimeshafanya hivyo.
“Endapo
itashindwa kuthibitisha ndani ya muda unaotakiwa tutachukua hatua ya kuiweka
timu nyingine badala ya El Merriekh kwani tunahitaji kuwa na mashindano yenye
ushindani wa kweli mwaka huu na bora zaidi kuliko miaka mingine,” alisema
Musonye raia wa Kenya.
Baadhi ya
timu nyingine ambazo si kutoka ukanda wa Cecafa ambazo zinatarajiwa kujumuishwa
kwenye michuano ya Kagame msimu huu ni Vita Club ya DR- Kongo, Bloemfontein
Celtics, Platinum FC na Silver Stars FC zote za Afrika Kusini pamoja na Dynamos
ya Zimbabwe.
Michuano
mwaka huu ya Kagame inatarajiwa kuanzia kutimua vumbi Julai 14 mwaka huu huku
viwanja vya Taifa na Chamazi vikitumika kwenye michuano hiyo.
Kwa Tanzania
Bara timu zitakazoshiriki ni Yanga ambao ni Mabingwa wa tetezi, Simba na Azam huku
Kenya ikiwa na timu ya Tusker wakati Burundi
ikiwakilishwa na Atletico.
Aidha kwa
mara ya kwanza nchi ya Sudan Kusini nayo itawakilishwa na Wau Salam wakati, Zanzibar
ikiwa na kikosi cha Mafunzo, Uganda ikiwalishwa na URA na APR ikishiriki kwa
niaba ya Rwanda.
Timu
nyingine ni pamoja na Elman ya Somalia, Ports ya Djibouti, Red Sea ya Eritrea
na mabingwa wa Ethiopia Coffee. Msimu uliopita, Yanga ilifunga Simba bao 1-0 na
kutwaa ubingwa katika mchezo wa fainali ulipigwa Julai 10 mwaka jana.