Kutoka ndandao wa Bin Zuber
KAMATI ya Uchaguzi ya klabu ya Yanga
ya Dar es Salaam, imemuengua mgombea nafasi ya Makamu Mwenyekiti, Ally Mayay
Temebele kwa sababu mbili; kwanza pingamizi alilowekewa na pili kuidharau
Kamati hiyo kwa kutofika kwenye usikilizwaji wa pingamizi lake bila ya taarifa
yoyote.
Katibu wa Kamati hiyo, Francis
Kaswahili ameambia BIN ZUBEIRY jioni hii kwamba pingamizi
alilowekewa Mayay lilistahili majibu yake, lakini kwa kuwa hakutokea Kamati
imeona mambo mawili, mtoa pingamizi ana hoja na pili Mayay ameidharau Kamati
hiyo kwa kutofika bila taarifa.
Kaswahili alisema pingamizi dhidi ya
‘Meja’ Mayay, Nahodha wa zamani wa Yanga lilikuwa kuhusu kushindwa kutekeleza
majukumu yake awali, akiwa kiongozi wa klabu hiyo na ndani ya muda mfupi
anaomba tena uongozi.
“Wagombea wengine wote wamepitishwa
kuendelea na usajili kwa ajili ya uchaguzi, isipokuwa Ally Mayay pekee,”alisema
Kasawahili.
Kuenguliwa kwa Mayay, kunafanya
nafasi ya Makamu Mwenyekiti ibakiwe na watu watatu, ambao ni Ayoub Nyenzi, Yono
Kevela na Clement Sanga, wakati wagombea Uenyekiti ni Yussuf Mehboob Manj, John
Jambele, Edgar Chibura na Sarah Ramadhani.
Katika nafasi za Ujumbe ni Lameck
Nyambaya, Ramadhani Mzimba ‘Kampira’, Mohamed Mbaraka, Ramadhani Said, Edgar
Fongo, Beda Simba, Ahmad Gao, Mussa Katabaro, George Manyama, Aaron Nyanda,
Abdallah Bin Kleb, Omary Ndula, Shaaban Katwila, Jumanne Mohamed Mwammenywa,
Abdallah Mbaraka, Peter Haule, Justin Baruti na Abdallah Sharia.
Awali, Mkuu wa Wilaya ya Handeni,
Muhingo Rweyemamu, Mfanyabiashara Muzamil Katunzi na Katibu Mkuu wa Wizara ya
Madini, Eliakhim Masu walichukua fomu za kugombea Ujumbe lakini wakashindwa
kurudisha, wakati Isaac Chanzi pia hakurudisha fomu ya Makamu Mwenyekiti hivyo
moja kwa moja hao hawamo katika kinyang’anyiro.
Uchaguzi huo, unaokuja baada ya
Wajumbe wengi wa Kamati ya Utendaji katika uongozi uliokuwa madarakani, akiwemo
Mwenyekiti Wakili Lloyd Baharagu Nchunga na Makamu wake, Davis David Mosha
kujiuzulu utafanyika Julai 15, mwaka huu Dar es Salaam.
Mapema jana, Mwenyekiti wa Kamati ya
Uchaguzi ya klabu hiyo, walipokea pingamizi dhidi ya wagombea Uenyekiti, Manji
na Sarah Ramadhani, Makamu Mwenyekiti, Yono Kevella, Clement Sanga na Ally
Mayay.
Lakini Jaji Mkwawa amesema Kamati
yake inaweza kusikiliza na kuamua kuhusu mapingamizi hayo bila ya kuwepo
waliowekewa au walioweka, ila tu amesistiza ni vema wakawepo ili watetee hoja
zao.
Aidha, kuhusu tamko la mwanachama
Abeid Abeid ‘Falcon’ kutaka ufafanuzi wa Katiba ipi itatumika katika uchaguzi
huo, Jaji Mkwawa alisema itatumika Katiba ya mwaka 2010 iliyowasilishwa
Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) Juni 17, mwaka huo.
Amemtoa wasiwasi Abeid kwamba katiba
ya 2011 iliyokuwa na matatizo kiasi cha kupingwa mahakamani na wanachama wa
klabu hiyo haitatumika.
Lakini pia, Mkwawa amesema pamoja na
kwamba uchaguzi huu unakuja baada ya Wajumbe wengi wa Kamati ya Utendaji,
wakiwemo Mwenyekiti na Makamu wake kujiuzulu, Wajumbe waliojiuzulu kutoka
kwenye uongozi huo wanaruhusiwa kugombea.
Aidha, kuhusu wagombea kusaidia
klabu katika masuala yanayohusu fedha katika kipindi hiki kigumu, Jaji Mkwawa
amesema hayana matatizo yakifanyika katika taratibu zinazoeleweka.
0 comments:
Post a Comment