TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
MAAMUZI KUHUSU RUFAA
DHIDI YA MAAMUZI YA KAMATI ZA UCHAGUZI VYAMA VYA MPIRA WA MIGUU MKOA WA
MBEYA (MREFA), MKOA WA SHINYANGA (SHIREFA) NA MKOA WA DAR ES SALAAA
(DRFA).
19 OKTOBA 2012
1. Kwa mujibu wa Katiba ya TFF Ibara ya 49(1), Kanuni za Uchaguzi za wanachama wa TFF, Ibara ya 10(6), 12(1) na 26(2) na (3), Kamati ya Uchaguzi ya TFF katika
vikao vyake vilivyofanyika tarehe 12 na 18 Oktoba 2012 ilijadili
michakato ya chaguzi za vyama vya mpira wa miguu vya Mikoa ya Mbeya
(MREFA), Shinyanga (SHIREFA) na Dar es Salaam (DRFA) na kutoa maamuzi kama ifuatavyo:
(a) Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Mbeya (MREFA)
(i) Rufaa ya Ndg. Charles Makwaza: Kamati ilijadili rufaa iliyowasilishwa na Ndg. Charles Makwaza dhidi
ya Kamati ya Uchaguzi ya MREFA, iliyoomba Kamati ya Uchaguzi ya TFF
kubatilisha uamuzi wa Kamati ya Uchaguzi ya MREFA kumpitisha Ndg. John
Mwamwaja kugombea nafasi ya Mwenyekiti wa MREFA, kwamba hakutekeleza
wajibu wa kikatiba wa kuitisha Mkutano Mkuu wa MREFA kwa muda wa miaka
3.
Baada ya kupitia maelezo ya warufani na warufaniwa, Kamati ya Uchaguzi ya TFF ilijiridhisha kuwa vielelezo na maelezo ya Ndg. Charles Makwaza yaliyowasilishwa mbele ya Kamati kwa kiwango kikubwa hayakuwa ya kweli. Kamati ya Uchaguzi ya TFF imeitupa rufaa hiyo.
(ii) Rufaa ya Ndg. Lusekelo E. Mwanjala: Kamati ilijadili rufaa iliyowasilishwa na Ndg. Lusekelo E. Mwanjala ikipinga maamuzi ya Kamati ya Uchaguzi ya MREFA
kuliondoa jina lake kugombea nafasi ya Mwenyekiti wa MREFA, kwa kigezo cha kutokuwa na uzoefu wa uongozi wa mpira wa Miguu.
Kamati
ilipitia vielelezo kuhusu rufaa na kujadili maelezo ya Mrufani na
Mrufaniwa na ilijiridhisha kuwa Ndg. Mwanjala anakidhi kigezo cha
uzoefu. Kamati inakubaliana na rufaa ya mrufaa dhidi ya maamuzi ya Kamati ya Uchaguzi ya MREFA na hivyo imemrejesha Ndg. Mwanjala kugombea nafasi ya Mwenyekiti wa MREFA.
(iii) Rufaa ya Ndg. Thadeo T. Kalua: Kamati ilijadili rufaa iliyowasilishwa mbele yake na Ndg. Kalua ikipinga maamuzi ya Kamati ya
Uchaguzi ya MREFA kuliondoa jina lake kugombea nafasi
ya Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa TFF, kwa kigezo cha kutokuwa Mkazi wa Mkoa
wa Mbeya. Kamati ilipitia vielelezo kuhusu rufaa hii na kubaini kuwa
Katiba ya MREFA iliyosajiliwa haina sharti hilo kwa waombaji uongozi. Kamati inakubaliana na maombi ya
(iv) mrufaa na inamrejesha Ndg. Thadeo Kalua kugombea nafasi ya Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa TFF.
(v) Uchaguzi wa MREFA utafanyika Jumamosi, tarehe 27 Oktoba 2012 kama ulivyopangwa.
(b) Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Shinyanga (SHIREFA).
(i) Rufaa ya Ndg. Ibrahim Magoma: Kamati ilijadili rufaa iliyowasilishwa na Ndg. Magoma ikipinga maamuzi ya Kamati
ya Uchaguzi ya SHIREFA kuliondoa jina lake kugombea nafasi ya Katibu wa
SHIREFA, kwa kigezo cha kuingilia Mchakato wa Uchaguzi kunyume na
Kanuni za Uchaguzi za
wanachama wa TFF na pia kutozingatia matakwa ya Kanuni hizo katika
kujaza fomu za maombi ya uongozi wa SHIREFA.
Kamati
ilipitia vielelezo kuhusu rufaa ya Ndg. Magoma na kujadili maelezo ya
Mrufani na Mrufaniwa na ilijiridhisha kuwa Ndg. Magoma aliingilia
mchakato wa uchaguzi wa SHIREFA kunyume na Kanuni za Uchaguzi za
wanachama wa TFF akiwa Katibu Mkuu wa SHIREFA kwa kushiriki kuivunja
Kamati ya Uchaguzi ya SHIREFA iliyokuwa ikendelea na mchakato wa
uchaguzi wa SHIREFA. Kamati inakubaliana na uamuzi wa Kamati ya Uchaguzi ya SHIREFA wa kumwondoa Ndg. Magoma kugombea nafasi ya Katibu wa SHIREFA. Kamati ya Uchaguzi ya TFF imeitupa rufaa hiyo.
(ii) Uchaguzi wa SHIREFA umesogezwa Mbele kwa siku nne. Uchaguzi huo utafanyika Alhamisi, tarehe 25 Oktoba 2012, mjini Shinyanga.
(c) Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es salaam (DRFA).
Kamati ya Uchaguzi ya TFF ilijadili Mchakato wa Uchaguzi wa DRFA na rufaa dhidi ya maamuzi ya Kamati ya Uchaguzi ya DRFA na kuamua kama ifuatavyo:
(i) Marekebisho na usajili wa Katiba ya DRFA:
Hoja ya rufaa iliwasilishwa na Ndg. Michael R. Wambura ilikihoji
uhalali wa marekebisho na usajili wa Katiba ya DRFA, kwamba
usajili wa Katiba ya DRFA si halali. Kamati ilibaini kuwa marekebisho
ya Katiba hiyo yalifanyika kwa kufuata maagizo ya TFF na kwamba DRFA
ilizingatia maagizo hayo. Kamati ya Uchaguzi ya TFF iliridhika kuwa
Katiba ya DRFA imesajiliwa na Msajili wa vyama na vilabu vya michezo
baada ya kuridhiwa na TFF, na hivyo, Kamati iliitupa hoja hiyo ya Mrufani kuhusu uhalali na usajili wa Katiba ya DRFA.
(ii) Kuundwa kwa Kamati ya Uchaguzi ya TFF :
Hoja ya rufaa ya Ndg. Michael R. Wambura iliomba Kamati ya Uchaguzi ya
TFF kutoa tamko kuwa Kamati ya Uchaguzi ya DRFA imeundwa bila
kufuata Kanuni za Uchaguzi Ibara ya 3(2). Kamati iliridhika kuwa Kamati
ya Uchaguzi ya DRFA iliteuliwa kabla ya marekebisho ya Kanuni za
Uchaguzi za wanachama wa TFF hususan, Ibara ya 3(2), hivyo uteuzi wa wajumbe wa Kamati hiyo haukukiuka Kanuni za Uchaguzi. Kamati iliitupa rufaa hiyo.
(iii) Wapiga kura wa Mkutano Mkuu wa DRFA: Hoja za rufaa za Ndg. Michael R. Wambura na Ndg. Juma Jabir ziliomba
kuyaondoa majina ya Ndg. Abeid Mziba, Ndg. Salehe Ndonga, Peter Muhinzi
na Ndg. Daudi Kanuti katika orodha ya wapiga kura wa Mkutano Mkuu wa
DRFA na uongozi wa wanachama wa DRFA, kwamba hawana sifa kwa mujibu wa
Kanuni za Uchaguzi na Katiba za wanachama wa DRFA. Kamati ya Uchaguzi ya
TFF haikupata vielelezo kuhusu hoja iliyowasisilishwa mbele ya Kamati
na hivyo kuitupa hoja hiyo ya mrufani.
(iv) Rufaa dhidi ya Ndg. Mohamed Salim (Bakhressa) kugombea nafasi ya Mwenyekiti wa DRFA. Rufaa dhidi ya uamuzi wa Kamati ya Uchaguzi ya
DRFA wa kumpitisha Ndg. Amin Mohamed Salim (Bakhressa) kugombea nafasi ya Mwenyekiti wa DRFA iliyowasilishwa na Ndg. Michael R. Wambura na Ndg. Juma Jabir iliomba
jina la Ndg. Amin Mohamed Salim (Bakhressa) liondolewe katika orodha ya
wagombea uongozi wa DRFA kwa nafasi ya Mwenyekiti, kwa kuwa hana elimu
ya kiwango cha kidato cha nne na hivyo kutokidhi matakwa ya Katiba ya
DRFA Ibara ya 29(2) inayotamka kwamba ‘Mtu yeyote
anayegombea nafasi yoyote ya DRFA hana budi awe na kiwango cha elimu
kisichopungua kidato cha nne (Academic Certificate of
Ordinary Secondary Education).
Kamati
ya Uchaguzi ya TFF ilipitia vielelezo kuhusu rufaa dhidi ya maamuzi ya
Kamati ya Uchaguzi ya DRFA na kujadili maelezo ya Warufani, Kamati ya
Uchaguzi ya DRFA na Ndg. Amin Mohamed Salim na ilijiridhisha kuwa Ndg.
Amin Mohamed Salim (Bakhressa) hana elimu ya kiwango cha kidato cha nne
na hivyo hakidhi matakwa ya Katiba ya DRFA Ibara 29(2). Kwa kutokidhi
matakwa hayo ya katiba ya DRFA, Ndg. Amin Mohamed Salim (Bakhressa)
hastahili kugombea nafasi ya Mwenyekiti wa DRFA. Kamati ya Uchaguzi ya TFF inakubaliana na maombi ya Warufaa.
(v) Rufaa kupinga kuenguliwa kugombea Uongozi DRFA: Ndg. Evans Elieza na Ndg. Juma Jabir waliwasilisha rufaa wakiomba
Kamati ya Uchaguzi ya TFF kutengua uamuzi wa Kamati ya Uchaguzi ya DRFA
wa kuwaengua kugombea uongozi kwa madai ya kugushi sahihi ya Katibu wa
Chama cha Mpira wa Miguu Wilaya ya Kinondoni (KIFA). Katika vielelezo
mbalimbali vilivyoletwa mbele ya Kamati na baada ya kuwahoji warufani,
Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya DRFA, Katibu wa KIFA, Ndg. Seif Ally Mailo aliyeshuhudia
maelezo ya fomu za waombaji uongozi DRFA na baadhi ya waombaji uongozi
ambao kupitishwa kwao na Kamati ya Uchaguzi ya DRFA kulilalamikiwa,
Kamati ilibaini kuwa kulikuwa na ukiukwaji mkubwa wa Kanuni na taratibu
za uchaguzi zilizofanywa na Kamati ya Uchaguzi ya DRFA na pia ama KIFA
au wagombea wenyewe. Kutokana na
mkanganyiko, maelezo yenye utata kutoka kwa warufani na warufaniwa na
maamuzi ya utata ya Kamati ya Uchaguzi ya DRFA yameufanya mchakato wa
uchaguzi wa DRFA kupoteza hadhi ya uchaguzi unaozingatia Kanuni za
Uchaguzi na misingi ya demokrasia na uwazi kama ilivyoainishwa kwenye
Kanuni za Uchaguzi za TFF. Kamati ya Uchaguzi ya TFF ilijiridhisha
kwamba:
· Kamati
ya Uchaguzi ya DRFA iliwapitisha wagombea Ndg. Gungurugwa Tambaza, Ndg.
Mohammed Bhinda, Ndg. Benny Kisaka na Ndg. Hamisi Ayoub Mpapai bila
kuwa na vielelezo vinavyothibitisha kuwa wana kiwango cha elimu
kisichopungua kidato cha nne (Academic Certificate of Ordinary Secondary Education).
· Hoja ya kughushi saini ya Katibu wa KIFA katika kushuhudia maelezo ya baadhi ya wombaji uongozi, ambayo ilitumiwa na Kamati ya Uchaguzi ya DRFA kuwaondoa kugombea uongozi waombaji uongozi watano (5) Ndg. Hamis Ambar, Ndg. Hamisi Kisiwa, Ndg. Andrew Tupa, Ndg. Evans Elieza na Ndg. Juma
Jabir haikutumika kuwaondoa baadhi wagombea ingawa fomu za waombaji uongozi saba zilisainiwa na Ndg. Ndg. Seif Ally Mailo.
· Ndg. Seif
Ally Mailo ambaye si mwajiriwa na si kiongozi wa KIFA hakuwa na mamlaka
ya kushuhudia maelezo ya wagombea kwa mujibu wa Kanuni za Uchaguzi.
· Kulikuwa na hali ya kumficha Ndg. Seif
Ally Mailo aliyesaini fomu za wagombea walioenguliwa kwa kigezo cha
kughushi saini asifike kwenye kamati ya Uchaguzi ya TFF kutoa maelezo
kuhusu ushiriki wake katika mchakato wa uchaguzi
wa DRFA.
· Fomu
za wagombea Ndg. Said H.Tully na Ndg. Shaffih Dauda zilizojadiliwa na
Kamati ya Uchaguzi ya DRFA na hivyo kupitishwa na Kamati hiyo
zilichezewa (tempered-with) kwa kunyofolewa baadhi ya kurasa na kuwekwa
kurasa zenye maelezo na saini ambazo si za Ndg. Said H.Tully na Ndg.
Shaffih Dauda. Wagombea hao ambao walikuwa wamepetishwa na Kamati ya
Uchaguzi ya DRFA kwa maelezo kwamba fomu zao zilikuwa zimeshudiwa kwa
sahihi halali ya Ndg. Ndg. Seif Ally Mailo
walikana
kwa maandishi na kutoa vielelezo vilivyothibitisha kwamba fomu zao
zilichezewa na maelezo yaliyo kwenye kurasa zilizobadilishwa siyo wao
walioyandika na kusaini.
· Kamati
ya Uchaguzi ya DRFA iliwaondoa baadhi ya waombaji uongozi kwa maelezo
kwamba maelezo kwenye fomu za wagombea hao hayakushuhudiwa na viongozi
vyama wanachama wa DRFA wenye mamlaka ya kushuhudia maelezo ya waombaji
uongozi lakini bila kuzingatia matakwa hayo ya kikanuni ikawapitisha
kugombea Ndg. Muhsin S. Balhabou na Ndg. Benny Kisaka ambao maelezo ya
kwenye fomu zao hayakushuhudiwa na kiongozi wa chama mwanachama
yeyote wa DRFA.
· Kamati
ya Uchaguzi ya DRFA inahusika kwa kiwango kikubwa katika ukiukwaji wa
Kanuni na taratibu za uchaguzi na kutozingatia matakwa ya Katiba ya DRFA
katika mchakato wa uchaguzi wa viongozi wa DRFA.
Kamati ya Uchaguzi ya TFF kwa kuzingatia Katiba ya TFF Ibara ya 49(1), Kanuni za Uchaguzi za wanachama wa TFF Ibara ya 10(6), 12(1) na 26(2) na (3):
(i) Imeifuta
Kamati ya Uchaguzi ya DRFA. DRFA inaagizwa kuteuwa Kamati mpya ya
Uchaguzi itakayoandaa na kutekeleza majukumu yake ikizingatia Kanuni za
Uchaguzi za wanachama wa TFF na Katiba ya DRFA. Uteuzi wa Kamati mpya ya
Uchaguzi ya DRFA ufanyike kabla ya tarehe 25 Oktoba 2012
(ii) Imefuta
mchakato wa Uchaguzi wa DRFA. Mchakato wa uchaguzi utaanza upya tarehe
29 Oktoba 2012 na uchaguzi utafanyika tarehe 08 Desemba 2012.
Wagombea wote waliokuwa wamelipia Fomu za maombi ya uongozi (Fomu Na.
1) wanaokidhi sifa za kugombea
uongozi kwa mujibu wa Katiba ya DRFA na Kanuni za Uchaguzi za wanachama
wa TFF wajaze upya Fomu Na.1 bila kutozwa ada kwa nafasi zinazoendana
na zile walizokuwa wameomba kugombea.
Deogratias Lyatto
MWENYEKITI
KAMATI YA UCHAGUZI TFF
0 comments:
Post a Comment