Thursday, October 18, 2012

SIMBA NA KAGERA HAKUNA MBABE





TIMU ya Simba jana ilitoka sare ya 2-2 na Kagera Sugar katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kwenye mchezo uliochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Kwa matokeo hayo, Simba imefikisha pointi 18 na kuendelea kuongoza Ligi Kuu, kutokana na Azam FC kulazimishwa sare ya bila kufungana na Prisons kwenye Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya.

Hadi mapumziko, Simba SC walikuwa mbele kwa bao 1-0, lililotiwa kimiani na mshambuliaji wa kimataifa raia wa Zambia, Felix Mumba Sunzu Jr. dakika ya nane, akiunganisha kwa kichwa krosi ya Nassor Masoud ‘Chollo’ kutoka wingi ya kulia.

Kipindi cha pili Simba ilirudi na moto tena na katika dakika ya 51, Mrisho Khalfan Ngassa aliifungia timu hiyo bao la pili kwa shuti kali lililowababatiza mabeki wa Kagera Sugar kutinga nyavuni.

Baada ya hapo, Kagera walizinduka na kuanza kulishambulia lango la Simba kupitia pembeni na dakika ya 64 Themi Felix aliunganisha kwa kichwa krosi ya George Kavilla na kuifungia Kagera bao la kwanza.

Bao liliwazindua Kagera, ambao waliongeza kasi ya kushambulia lango la Simba na dakika ya 66, Juma Nyosso alimkwatua kwenye eneo la penalti Paul Ngwai na Salum Kanoni akaenda kupiga penalti, akiisawazishia Kagera.

Baada ya hapo timu zilianza kushambuliana kwa zamu na mpira ulikuwa mzuri zaidi kutokana na mashambulizi ya pande zote mbili.

Katika mechi nyingine, Mgambo imeifunga Toto African 2-0 kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.

JKT Ruvu imezinduka baada ya kuifunga Polisi Morogoro 2-0 kwenye Uwanja wa Jamhuri, Morogoro

JKT Oljoro imetoka 0-0 na African Lyon.

Simba SC; Juma Kaseja (Nahodha), Nassor Masoud ‘Chollo’, Amir Maftah, Paschal Ochieng, Juma Nyosso, Mwinyi Kazimoto, Amri Kiemba, Haruna Moshi, Felix Sunzu, Emmanuel Okwi na Mrisho Ngassa.

Kagera Sugar; Andrew Ntala, Salum Kanoni, Martin Muganyizi, Amandus Nesta (Nahodha), Benjamin Effe, Malegesi Mwangwa, Daudi Jumanne, George Kavilla, Shijja Mkina, Enyinna Darlington na Wilfred Ammeh.

0 comments: