Kamati
ya Ligi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) ilikutana jana
(Oktoba 5 mwaka huu) kupitia na kufanya uamuzi katika masuala mbalimbali
na kupanga Ligi Daraja la Kwanza (FDL) ianze kutimua vumbi Oktoba 20
mwaka huu.
Timu
zimepangwa katika makundi matatu ya timu nane nane ambapo zitacheza
ligi hiyo kwa mtindo wa nyumbani na ugenini. Mshindi wa kila kundi ndiye
atakayepata tiketi ya kucheza Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) msimu ujao
wakati timu ya mwisho kila kundi itashuka daraja kurudi Ligi ya Mkoa.
Kundi
A lina timu za Burkina Moro ya Morogoro, Kurugenzi Mufindi ya Iringa,
Majimaji ya Songea, Mbeya City ya Mbeya, Mlale JKT ya Ruvuma, Mkamba
Rangers ya Morogoro, Polisi Iringa na Small Kids ya Rukwa.
Ndanda
FC ya Mtwara, Ashanti United, Green Warriors, Moro United, Polisi,
Tessema, Transit Camp na Villa Squad zote za Dar es Salaam ndizo
zinazounda kundi B wakati kundi C ni Kanembwa JKT ya Kigoma, Morani ya
Manyara, Mwadui ya Shinyanga, Pamba ya Mwanza Polisi Dodoma, Polisi
Mara, Polisi Tabora na Rhino Rangers ya Tabora.
Ada
ya ushiriki wa ligi ni sh. 200,000 zinazotakiwa kulipwa kabla ya Oktoba
13 mwaka huu. Pia Oktoba 13 mwaka huu kutakuwa na kikao kati ya
wenyeviti wa klabu zote zinazoshiriki ligi hiyo na Kamati ya Ligi ambapo
pia itafanyika draw (ratiba).
MECHI YA KAGERA SUGAR, YANGA YASOGEZWA
Kamati
ya Ligi imesogeza mbele kwa siku moja mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom kati
ya Kagera Sugar na Yanga iliyokuwa ichezwe kesho (Oktoba 7 mwaka huu)
mjini Bukoba kutokana na Uwanja wa Kaitaba kuwa na shughuli nyingine za
kijamii.
Sasa
mechi hiyo itachezwa Jumatatu (Oktoba 8 mwaka huu) kwenye uwanja huo
huo. Mabadiliko hayo pia yameathiri mechi kati ya Toto Africans na Yanga
iliyokuwa ichezwe Oktoba 10 mwaka huu Uwanja wa CCM Kirumba jijini
Mwanza. Mechi hiyo sasa itachezwa Oktoba 11 mwaka huu.
WAAMUZI WATATU WAONDOLEWA, SIMBA YAPIGWA FAINI
Kamati
ya Ligi imewaondoa waamuzi watatu wa Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kwa
kushindwa kumudu michezo waliyopangiwa. Waamuzi hao ni Mathew Akrama wa
Mwanza aliyechezesha mechi namba 80 ya Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kati ya
Yanga na Simba iliyochezwa Oktoba 3 mwaka huu.
Wengine
ni Paul Soleji wa Mwanza aliyechezesha mechi kati ya Simba na Tanzania
Prisons, na mwamuzi msaidizi namba mbili kwenye mechi hiyo Mwarabu Mumbi
wa Morogoro. Pia mwamuzi msaidizi namba mbili wa mechi ya Yanga na
Simba, Ephrony Ndissa wa Dar es Salaam amepewa onyo.
Kamishna
wa mechi namba 28 kati ya Yanga na African Lyon, Pius Mashera
ameondolewa kwenye orodha ya makamishna wa ligi hiyo kwa kuchelewa
kufika kwenye kikao cha maandalizi ya mechi (Pre match meeting) na
uwanjani.
Vilevile
Mashera kwenye ripoti yake aliwasilisha malalamiko dhidi ya msimamizi
wa kituo cha Dar es Salaam, na kwa vile suala hilo ni la kinidhamu
ametakiwa alipeleke kwenye Kamati ya Nidhamu na Usuluhishi ya TFF.
Nayo
Simba imepigwa faini ya jumla ya sh. 600,000 kwa kuchelewa kufika
kwenye pre match meeting ya mchezo wao dhidi Tanzania Prisons (sh.
100,000) na kwa washabiki wake kuwatupia chupa za maji waamuzi wa mechi
hiyo (500,000).
Pia
Kamati ya Ligi imeagiza kuwa kwa vile suala la kipa Shabani Kado wa
Mtibwa Sugar kudaiwa kumpiga kiongozi mmoja wa Ruvu Shooting mara baada
ya mechi kati ya timu hizo iliyochezwa Uwanja wa Azam Complex ni la
kinidhamu lipelekwe kwenye Kamati ya Nidhamu na Usuluhishi ya TFF.
YANGA, AFRICAN LYON KUTOVAA BEJI YA MDHAMINI
Kwa
vile msimu huu mdhamini mwenyewe ndiye anayegawa vifaa kwa timu, Kamati
ya Ligi imeagiza Vodacom iandikiwe barua na nakala kwa klabu zote ili
kujua timu ambazo tayari zimekabidhiwa vifaa hivyo zikiwemo logo na siku
ambapo timu husika zilipokea.
Baada
ya majibu ya Vodacom ndipo Kanuni za Ligi Kuu zitakapotumika kutoka
adhabu kwa timu ambazo zitabainika kuwa zilipokea vifaa lakini
hazikuvitumia.
Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
0 comments:
Post a Comment