Mchezo
wa Ligi Kuu ya Vodacom kuwania ubingwa wa Tanzania Bara kati ya Yanga
na Ruvu Shooting uliopangwa kuchezwa kesho (Oktoba 20 mwaka huu) Uwanja
wa Chamazi sasa umehamishiwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuanzia saa
10.15 jioni.
Mabadiliko
hayo yamefanyika kutokana na maombi ya timu hizo mbili kutaka mechi
ichezwe Uwanja wa Taifa kutokana na sababu mbalimbali ambazo zimeridhiwa
na Kamati ya Ligi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
ikiwemo siku hiyo uwanja huo kutokuwa na mechi.
Viingilio
katika mechi hiyo itakayokuwa chini ya mwamuzi Amon Paul kutoka Mara ni
sh. 5,000 viti vya kijani na bluu, sh. 8,000 viti vya rangi ya chungwa,
sh. 15,000 VIP B na C na sh. 20,000 kwa VIP A.
Pia
Kamati ya Ligi imekataa ombi la timu ya Azam kutaka mechi zake za
nyumbani za ligi hiyo zichezwe dhidi ya Simba na Yanga zichezwe Uwanja
wa Chamazi kutokana na sababu za kiusalama.
Nayo
Coastal Union itakuwa mwenyeji wa Mtibwa Sugar katika mechi nyingine ya
ligi hiyo itakayochezwa kesho (Oktoba 20 mwaka huu) katika Uwanja wa
Mkwakwani jijini Tanga.
Mchezo
huo namba 56 wa kukamilisha raundi ya nane utachezeshwa na mwamuzi
Israel Nkongo atakayesaidiwa na Hamis Chang’walu na Omari Kambangwa,
wote kutoka Dar es Salaam.
Ligi
hiyo itaendelea tena Jumapili (Oktoba 21 mwaka huu) kwa mechi tatu. JKT
Ruvu itaoneshana kazi na Oljoro JKT kwenye Uwanja wa Chamazi, Mgambo
Shooting itaikaribisha Simba kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga
wakati Tanzania Prisons na Toto Africans zitapimana ubavu kwenye Uwanja
wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya.
TWFA YATAKA ORODHA YA WAPIGA KURA
Kamati
ya Uchaguzi ya Chama cha Mpira wa Miguu wa Wanawake Tanzania (TWFA)
chini ya Mwenyekiti wake Ombeni Zavala imewataka wanachama wa TWFA ambao
ni mikoa ya Tanzania Bara kuwasilisha orodha ya wajumbe wao wa mkutano
wa uchaguzi.
Wajumbe
wenye sifa ya kuhudhuria Mkutano wa TWFA ni kutoka vyama vya mikoa
ambavyo tayari vimefanya uchaguzi. Wajumbe hao ni Mwenyekiti, Katibu na
Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa TWFA.
Mikoa
ambayo imeshafanya uchaguzi mpaka sasa ni Iringa, Kigoma, Mwanza, Pwani
na Tanga. Mikoa ambayo bado inahimizwa kufanya uchaguzi, na mwisho wa
kutuma majina ya wajumbe kwa Mwenyekiti Zavala ni Oktoba 25 mwaka huu.
Mkoa ambao utakuwa haujafanya uchaguzi utakuwa umenyimwa haki ya kushiriki uchaguzi wa TWFA utakaofanyika Novemba 4 mwaka huu.
MTANZANIA AOMBEWA ITC ACHEZE MAREKANI
Mchezaji
Millan Mbise kutoka Tanzania ameombewa Hati ya Uhamisho wa Kimataifa
(ITC) itakayomwezesha kucheza mpira wa miguu nchini Marekani.
Shirikisho
la Mpira wa Miguu la Marekani (USSF) limemuombea hati hiyo Mbise kama
mchezaji wa ridhaa ili ajiunge na timu ya Virginia Youth Soccer.
Klabu
ya zamani ya Mbise aliyezaliwa Agosti 18, 1994 imetajwa kuwa Super
Sport FC, na mechi ya mwisho kwenye timu hiyo alicheza Novemba 15 mwaka
juzi.
Shirikisho
la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) linafanya mawasiliano na pande husika
kabla ya kutoa hati hiyo kwa mchezaji huyo kama ilivyoombwa na
shirikisho hilo la Marekani.
TASMA WAANZA MCHAKATO WA UCHAGUZI
Chama
cha Madaktari wa Tiba ya Michezo Tanzania (TASMA) leo (Oktoba 19 mwaka
huu) kimetangaza kuanza mchakato wa uchaguzi wa chama hicho uliopangwa
kufanyika Novemba 28 mwaka huu.
Kwa
mujibu wa Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya TASMA, Dk. Francis
Mchomvu, fomu kwa wanamichezo wanaotaka kugombea uongozi wa chama hicho
zitaanza kutolewa Oktoba 21 mwaka huu.
Mwisho
wa kuchukua na kurejesha fomu hizo zinazopatikana ofisi za Shirikisho
la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) ni saa 10.00 alasiri ya Oktoba 26 mwaka
huu. Ada ya fomu kwa nafasi nne za juu ni sh. 200,000 wakati kwa nafasi
nyingine zilizobaki ni sh. 100,000. Kati ya Oktoba 27-31 mwaka huu
Kamati ya Uchaguzi ya TASMA itapitia fomu na kutangaza majina ya
waliojitokeza kuomba uongozi.
Nafasi
zitakazogombewa ni Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti, Katibu Mkuu, Katibu
Msaidizi, Mhazini, Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa TFF na wajumbe wawili wa
Kamati ya Utendaji.
Kipindi
cha pingamizi kwa waombaji ni kuanzia Novemba 1-6 mwaka huu, na
pingamizi zinatakiwa kuwasilishwa kwa Katibu wa Kamati ya Uchaguzi ya
TASMA kabla ya saa 10.00 alasiri ya Novemba 6 mwaka huu. Hakuna ada
kwenye pingamizi.
Pingamizi
zitajadiliwa na kufanyiwa uamuzi kati ya Novemba 7-9 mwaka huu. Usaili
utafanyika kati ya Novemba 10-11 mwaka huu ambapo matokeo ya usaili huo
vilevile yatatangazwa ili kutoa fursa kwa rufani ambazo zinatakiwa
kukatwa kati ya Novemba 11-13 mwaka huu.
Rufani
ambazo zinaambatana na ada y ash. 500,000 zinatakiwa kufikishwa kwa
Katibu Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kabla ya saa
10.00 alasiri ya Novemba 13 mwaka huu.
Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
0 comments:
Post a Comment