Friday, June 15, 2012

Cholo, Mweta waendelea kula bata Msimbazi


Na Mwandishi Wetu

UONGOZI wa Klabu ya Simba umesisitiza kuwa hauna mpango wa kumtema beki wa klabu hiyo, Nassor Said ‘Cholo’ pamoja na Wilbert Mweta katika usajili ujao wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara.

Msemaji wa Simba, Ezekiel Kamwaga amesema Simba wachezaji hao hawapo kwenye orodha wa wale watakaotemwa katika usajili  wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu ujao.

“Simba ina mipango mingi lakini katika usajili wake hatutawaacha nyota hao kama ambavyo wengi wanavyoamini kwa sababu hawapo kwenye orodha ya wale wataoachwa.

“Kama kuna taarifa za majeruhi  ni suala la ndani ya Simba na si busara kuliweka wazi, ila ninachosisitiza nikiwa ni kiongozi wa Simba kwamba Cholo na Mweta wataendela kuwepo klabuni msimu ujao wa ligi.

“Pia wakati wa kuwaacha wachezaji kwa ajili ya msimu ujao bado hivyo kauli za sasa kuwa tunamuwacha fulani na fulani anabakia si taarifa kutoka ndani ya Simba ambazo tunaziona kuwa na malengo mabaya na klabu yetu.
“Tunasema si sahihi kwa sababu wapo baadhi ya wachezaji waliomaliza mkataba na Simba lakini kutokana na umuhimu wao yapo mazungumzo yanayoendelea baina ya pande mbili hizi.

“Nichukue nafasi hii kuwasihi wanachana na wapenzi wa Simba kuwa makini katika wakati huu na wasiyumbishwe bali wasubiri taarifa rasmi itatolewa na uongozi,” alisema Kamwaga.

Cholo aloijiunga na Simba akitokea JKT Oljoro ya Arusha katika usajili wa ligi kuu msimu uliopita huku, Mweta akitua akitokea Toto Africans ya jijini Mwanza. Pamoja na usajili huo, Cholo ndiye aliyepata nafasi kubwa ya kucheza zaidi ya Mweta ambaye hakupata nafasi kutokana na uwepo wa kipa namba moja Juma Kaseja.

0 comments: