Tuesday, June 26, 2012

Ratiba ya Kagame hadharani




Na Mwandishi Wetu

RATIBA ya michuano ya Kombe la Kagame inatarajiwa kutolewa Ijumaa ijayo jijini Dar es Salaam ikiwa ni maandalizi ya michuano hiyo mikubwa kwa ngazi ya klabu katika Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.
Katibu Mkuu wa Baraza la vyama vya soka Afrika Mashariki Kati, (Cecafa) Nicholas Musonye  amesema kwamba, kabla ya kutolewa kwa ratiba hiyo itafanyika droo ya kupata makundi.

Aidha katibu huyo amesema kuwa, wanachosubiri hivi sasa ni uthibitisho wa klabu ya El Merriekh ya Sudan pekee, ambayo awali ilikuwa kwenye hatihati ya kutoshiriki michuano hiyo kutokana na sababu mbalimbali.

“Tunasubiri El Merreikh ambayo inatakiwa kuthibitisha ushiriki wao kwani klabu karibu zote zimeshafanya hivyo.

“Endapo itashindwa kuthibitisha ndani ya muda unaotakiwa tutachukua hatua ya kuiweka timu nyingine badala ya El Merriekh kwani tunahitaji kuwa na mashindano yenye ushindani wa kweli mwaka huu na bora zaidi kuliko miaka mingine,” alisema Musonye raia wa Kenya.

Baadhi ya timu nyingine ambazo si kutoka ukanda wa Cecafa ambazo zinatarajiwa kujumuishwa kwenye michuano ya Kagame msimu huu ni Vita Club ya DR- Kongo, Bloemfontein Celtics, Platinum FC na Silver Stars FC zote za Afrika Kusini pamoja na Dynamos ya Zimbabwe.

Michuano mwaka huu ya Kagame inatarajiwa kuanzia kutimua vumbi Julai 14 mwaka huu huku viwanja vya Taifa na Chamazi vikitumika kwenye michuano hiyo.

Kwa Tanzania Bara timu zitakazoshiriki ni Yanga ambao ni Mabingwa wa tetezi, Simba na Azam huku Kenya ikiwa na timu ya Tusker wakati Burundi  ikiwakilishwa na Atletico.

Aidha kwa mara ya kwanza nchi ya Sudan Kusini nayo itawakilishwa na Wau Salam wakati, Zanzibar ikiwa na kikosi cha Mafunzo, Uganda ikiwalishwa na URA na APR ikishiriki kwa niaba ya Rwanda.

Timu nyingine ni pamoja na Elman ya Somalia, Ports ya Djibouti, Red Sea ya Eritrea na mabingwa wa Ethiopia Coffee. Msimu uliopita, Yanga ilifunga Simba bao 1-0 na kutwaa ubingwa katika mchezo wa fainali ulipigwa  Julai 10 mwaka jana.

0 comments: